Waziri Mhagama alitaka Baraza la Uuguzi na Ukunga kusimamia Sheria na Miiko
Imewekwa tarehe: January 16th, 2025
Na WAF - Dodoma
WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amelitaka Baraza jipya la Wauguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) kuwachukulia hatua kali wauguzi na wakunga watakaokiuka misingi ya sheria na miiko ya taaluma zao.
Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati akizindua Baraza jipya la 63 la Uuguzi na Ukunga Tanzania, jijini Dodoma, wenye kauli mbiu isemayo “Wauguzi na Ukunga ni Watu Maalum kwa Kazi Maalum”.
"Baraza lenu lina kazi nyingi, miongoni mwa kazi zenu mnatakiwa kuhakikisha watumishi mnaowasimamia wanafanya kazi kwa weledi mkubwa ili kuwa na huduma zenye tija na ufanisi," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amelitaka Baraza hilo kuanzisha kanzi data inayoweza kufatilia wauguzi na wakunga wote nchini ili kurahisisha ufuatiliaji wa mienendo yao na upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Niwaelekeze Baraza, kuwa na mifumo mizuri inayohifadhi data za wauguzi na wakunga kuanzia walipo kwa sasa na mienendo yao, pia kuwatambua wauguzi na wakunga ambao hawana ajira ili kutengeneza mazingira mazuri ya kujiajiri kwa wataalam hao," amesema Waziri Mhagama.
Awali akimkaribisha Waziri wa Afya Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Bi. Ziada Sella amelitaka Baraza hilo kusimamia mawasiliano pamoja na lugha za staha kwa wananchi wanaowapatia huduma pamoja na kusimamia usajili wa wauguzi na wakunga sambamba na kutoa mafunzo mahala pa kazi kwa wataalam hao.
“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Baraza linaendela kusimamia mawasiliano na lugha nzuri kwa wataalam dhidi ya wananchi, eneo hili ni muhimu sana kwa sababu ndio matibabu yanaanzia hapo,” amesema Bi. Ziada
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Ukunga Tanzania Prof. Lilian Msele ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuteau wajumbe wa Baraza hilo na kuahidi kutekeleza kwa vitendo maelekezo yote aliyoyatoa Waziri Mhe. Mhagama.
“Nyuma ya mafanikio haya yote kuna mikono ya viongozi wetu kama Katibu Mkuu Dkt. John Jingu na Mganga Mkuu wa Serikali, wamekuwa mstari wa mbele kutushika mkono na kuhakikisha kila kwenye changamoto tunapata jawabu,” amesema Prof. Msele.