Binde Constantine Na Sifa Stanley
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, ametoa wito kwa vijana kuendelea kujitokeza kwa wingi kukopa mikopo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na Halmashauri.
Aliyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya vikundi vya wajasiriamali ambavyo ni Young Feders kilichopo Kata ya Miyuji na Tusumuke Agribusiness kutoka eneo la Nane Nane.
Wakati wa ziara hiyo Waziri alitoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo ambayo wataitumia kama mitaji ya kuendesha shughuli zao za ujasiriamali na kujikwamua kimaisha. “Waje kwenye ofisi za halmashauri, waje kwenye ofisi ya Waziri Mkuu ili wapatiwe mikopo lakini wahakikishe wanaitumia mikopo hiyo vizuri” alisema Waziri Jenista.
Aidha, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Asha Vuai aliahidi kutoa ushirikiano kwa wajasiriamali wenye uhitaji wa kupatiwa mikopo kwa ajili ya kuendeleza miradi yao. “Tunashukuru Waziri kwa kutenga muda wako na kutembelea vikundi, tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwenye ofisi yako kwa kuendelea kusimamia na kufuatilia vikundi vitakavyojitokeza kuomba mikopo” alisema Vuai.
Naye mwenyeketi wa kikundi cha Tusumuke Agribusiness Christopher Magesa, alisema kuwa, wapo tayari kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na ustadi mkubwa na kuwa mfano bora kwa vijana wengine. “tunao uwezo wa kuwa mfano bora kwa vijana wengine ndani ya nchi yetu katika kuonesha njia kwenye mradi huu wa kuku tunaoufanya” alisema Magesa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.