WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekagua visima vya dharura vinavyosafishwa, kufufuliwa na kuunganishwa katika mfumo wa usambazaji maji kwa wananchi na kuagiza zoezi hilo pamoja na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali liwe endelevu.
Majaliwa amekagua visima katika eneo la Tabata Relini na Mwananyamala Komakoma jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi, Novemba 10, 2022), ambapo ameshuhudia usafishwaji wa kisima pamoja na zoezi la usambazaji maji.
Visima hivyo ni miongozi mwa visima 197 vilivyochimbwa na Serikali mkoani Dar es Salaam ambapo kwa sasa 160 vimefufuliwa na kutoa lita milioni 29.4 kwa siku, Maji hayo yameunganishwa katika mfumo na hivyo kupunguza changamoto ya maji.
Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Bonde la Wami Ruvu pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) waendelee kufanya tafiti kubaini maeneo yenye maji mengi na kuchimba visima na kuyaingiza katika mfumo.
Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea
kulinda maeneo yote yenye vyanzo vya maji pamoja na kuyatumia vizuri maji yanayopatikana ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji hususani katika kipindi hiki cha ukame.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama
katika mikoa yote nchini likiwemo jiji la Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi.
Amewataka waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imedhamiria kuwatumikia.
Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini wizara imejipanga kuchimba mabwawa kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua na kuyaingiza katika mfumo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.