WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameipongeza Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na kuweza kuboresha Mawasiliano nchini.
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya miaka 10 ya UCSAF yaliyofanyika kwa siku nne katika Viwanja vya Nyerere Jijini Dodoma, Majaliwa alisema kuwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kushirikiana na watoa huduma mbalimbali wa Mawasiliano Nchini wameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kupeleka mawasiliano katika Kata 703, kwenye Vijiji 2501 na kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 5 pamoja na Mfuko huo kuweza kuchangia zaidi Shilingi Bilioni 118 katika kuhakikisha mawasiliano yanafika kwa wananchi.
“Mfuko huu tangu kuanzishwa kwake umetumia Shilingi bilioni 118 kufikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi zaidi ya milioni tano, kwa hiyo napenda kuwahahikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kupeleka mawasiliano maeneo yote ili kila mmoja aweze kunufaika na fursa hii” Alisema Majaliwa.
Majaliwa aliongeza kuwa, Mfuko umeweza kupeleka vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Shule 500 nchini pamoja na kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa Walimu zaidi ya 800 kwa lengo la kuwezesha wanafunzi kujifunza somo hilo kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alimpongeza Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Devis Mwamfupe na Mkurugenzi, Godwin Kunambi kwa jitihada zao za kuboresha mazingira ya wajasiriamali kufanya kazi zao.
Alitoa pongezi hizo baada ya kusoma bango lililoandaliwa na wafanyabiashara wadogo ‘machinga’ wa Dodoma kupongeza juhudi za serikali ya awamu ya tano.
“Pongezi kwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Mkurugenzi na Waheshimiwa Madiwani kwa kusimamia vizuri biashara katika Jiji la Dodoma” Alisema Majaliwa.
Majaliwa alisema kuwa wajasiriamali wa Dodoma wanapongeza juhudi za Rais Mhe. Dkt. John Magufuli za kuboresha mazingira ya wajasiriamali kutekeleza majukumu yao katika Jiji la Dodoma kutokana na uongozi mzuri wa viongozi wa Halmashauri hiyo.
Vilevile, Mhe. Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara hao kufanya biashara zao katika mazingira yanayokubalika.
“Machinga hakikisheni mazingira mnayofanyia biashara yanakuwa safi na wala msikae maeneo ambayo siyo rafiki kwa wateja wenu” alisema.
Kuhusu upimaji wa Afya, Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa Dodoma kujitokeza na kupima Afya zao ikiwemo hali ya Maambukizi ya Virusi vinavyosababisha Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) ili kupata matibabu mapema.
“Kila Mtanzania anawajibu wa kupima ili kutambua Afya yake na hii ni kampeni endelevu, nenda kituo cha afya kupima ili ujue afya yako…tunataka Watanzania wote tuwe tumefikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2020. Watanzania watakaogundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI wawe wameanza dawa za kufubaza virusi hivyo” alisema Majaliwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.