WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki Bunge Bonanza lililofanyika katika viwanja vya shule ya msingi na sekondari ya John Merlin ya jijini Dodoma ambapo ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wabunge na wananchi wengine washiriki katika michezo ili kuipa miili yao nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya kikazi.
“…Michezo kwetu sisi wabunge ni muhimu zaidi kwa sababu inatufanya tuwe na afya bora zaidi na pia michezo inasaidia watu kukutana pamoja na kuimarisha undugu, kujenga urafiki pamoja na kukuza vipaji. Nampongeza Spika Dkt. Tulia Ackson kwa ubunifu huu wa kuanzisha Bunge Bonanza ambalo litakuwa linafanyika mara kwa mara.”
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wabunge, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Watumishi wa Bunge pamoja na maafisa wengine wa Serikali walio shiriki katika bonanza hilo. Amesema bonanza lingine kama hilo linatarajiwa kufanyika Juni 24, 2023.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia amesema Bunge Bonanza litakuwa linafanyika mara nne kwa mwaka lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi umuhimu wa kushiriki katika kufanya mazoezi ili jamii iweze kuwa na afya bora zaidi.
Naye, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Katibu wa Michezo wa Baraza hilo Nassor Salim Ali (Jazeera) ambaye amemuwakilisha Spika wa Baraza la Wawakilishi amesema baraza litaendelea kushirikiana na Bunge ili kudumisha undugu kupitia michezo pamoja na shughuli mbalimbali wanazozifanya. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kudumisha Muungano.”
Awali, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza,Festo Sanga alisema pamoja na mambo mengine bonanza hilo limeanzishwa ili kumuunga mkono Rais Dkt. Samia ambaye amekuwa akiihamasisha jamii kushiriki katika kufanya mazoezi kwa ajili ya kuupa mwili afya na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Timu zilizoshiriki katika bonanza hilo ni timu ya Bunge na ya watumishi wa Bunge ambapo timu ya Bunge ilipata kombe la mshindi wa jumla baada ya kuishinda timu ya Watumishi wa Bunge katika michezo mingi. Michezo ni pamoja na mpira wa miguu, mpita wa wavu, mpita wa meza, mpira wa mikono, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kula chakula, kunywa soda, kuvuta kamba na kurusha tufe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.