WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuhusika na ulinzi wa watoto kwa kuweka mipango itakayoondoa mazingira yanayowafanya vijana balehe kuwa na tamaa ya vitu na kushawishika kujiingiza kwenye ngono katika umri mdogo.
“Suala la mimba za utotoni limekuwa mwiba kwa kipindi kirefu. Limekuwa likiwanyima wasichana wengi fursa ya kukamilisha malengo yao katika maisha. Hali hii haikubaliki lazima kila mmoja kwa nafasi yake aweke mikakati ya kuwawezesha watoto wa kike kumaliza masomo yao”.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Aprili 17, 2021) wakati wa uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe katika ukumbi wa Hoteli ya Morena, jijini Dodoma.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amesema programu za kuelimisha Vijana Balehe kuhusu madhara ya kuanza ngono mapema ziandaliwe ili washiriki kikamilifu katika masomo na masuala mengine ya maendeleo kwa kuwawezesha kupata taarifa sahihi.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha changamoto zinazolikabili kundi hilo zikiwemo za magonjwa ya kuambukizwa, upungufu wa taaluma sahihi za kujiajiri na kuajiriwa, matumizi ya dawa za kulevya, ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wadau wote wa masuala ya afya na maendeleo ya vijana balehe nchini kubuni na kuandaa afua zilizofanyiwa utafiti zenye kuleta matokeo chanya katika kutokomeza mimba za utotoni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.