Wadau mbalimbali watakiwa kutoa ushirikiano kwa kiwango cha juu katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kulifanya kuwa jiji bora na la kisasa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akizindua Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa Kambarage- Hazina jijini hapa.
Majaliwa amesema “ametoa wito kwa viongozi wa Mkoa wa Dodoma, Wizara, Halmashauri, Taasisi, sekta binafsi, Jumuiya za Kimataifa, wananchi na wadau wengine kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa Mpango Kabambe ili kufikia malengo ya kuwa na Jiji bora, lenye mandhari ya kuvutia na litakalokidhi mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya sasa na ya baadae”.
Aidha, ameutaka uongozi wa Jiji la Dodoma kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja pamoja na kusimamia kikamilifu udhibiti wa uendelezaji holela wa makazi. “Hatuhitaji kuona Jiji la Dodoma likiwa na makazi yasiyopimwa na holela. Wananchi hawawezi kuisubiri halmashauri bali halmashauri ndiyo inapaswa kuendana na kasi ya mahitaji ya wananchi. “Tayari katika baadhi ya maeneo wananchi wameanza na wanaendelea kujenga bila kufuata taratibu zinazotawala masuala ya ujenzi mijini” amesema Majaliwa. Matarajio ya Serikali ni kuona Jiji hilo lenye makazi yaliyopimwa, aliongeza.
Waziri Mkuu amelekeza kuwa upimaji wa maeneo uende pamoja na uendelezaji wa miundombinu na huduma muhimu katika maeneo yanayopimwa ikiwemo maji, umeme na barabara.
Aidha, ameliagiza Jiji la Dodoma kuweka utaratibu wa ufuatiliaji, utekelezaji na tathmini ya Mpango Kabambe ili kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wake. “Hili ni takwa la kisheria kwa mujibu wa kifungu namba 14 (3) cha Sheria ya Mipango Miji ya Mwaka 2007 ambacho kinaitaka kila mamlaka ya upangaji kutoa taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kabambe kila mwaka katika maeneo yao ya upangaji kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi” alisisiza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Dodoma ianzishe mchakato wa kutambua nyumba zote zilizojengwa kwenye barabara kwa lengo la kujua idadi kamili, uhalali wao kuwepo au kama ni wavamizi na baadaye kuandaa utaratibu wa fidia kwa wananchi wanaostahili.
Uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma ulifanyika mwaka 1973 ikiwa ni maelekezo ya Chama cha TANU kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma, kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na kushoto ni Mhe. Jenista Mhagama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuuanayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa (kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi ramani ya mpango kabambe wa Jiji la Dodoma. Katikati ni Naibu Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Emmanuel Chibago.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kuuzindua rasmi Mpango Kabambe wa Jiji la Dodooma
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.