WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza ufundishaji wa somo la Elimu kwa Michezo ufanyike kwa wanafunzi wote katika Shule za Msingi na kuhamasisha wanafunzi wa shule za Sekondari kusoma somo hilo.
Amesema kuwa hatua hiyo itawasaidia watoto kujenga moyo wa kujiamini, kuwa ubunifu, kuongeza mshikamano na umoja wa kitaifa pamoja na kuimarisha afya ya taifa.
Ametoa kaudli hiyo leo (Jumanne, Juni 8, 2021) alipofurngua mashindano ya michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari (UMISSETA) katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara.
Aliongeza kuwa vyuo vya ualimu vinapaswa kuimarisha masomo ya Elimu kwa michezo ili kila mhitimu aweze kutoka na ujuzi wa ufundishaji wa michezo na kutengeneza wataalamu wa kutosha ili kusaidia kukuza vipaji vya wanafunzi shuleni.
Amesema kuwa ili kupata wanamichezo na wasanii chipukizi wengi na bora ni lazima kuimarisha ufundishaji wa taaluma ya michezo kuanzia ngazi za awali, msingi, sekondari na vyuo.
“Kila ngazi ina umuhimu na kujenga msingi wa ngazi inayofuatia. Ndiyo sababu katika nchi zilizoendelea wangamichezo wake wengi wanaoshiriki michezo ya Kimataifa kama vile Michezo ya Olimpiki na Jumuia ya Madola ni Wanafunzi wa Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Tanzania tunayo hazina ambayo tukiitumia kikamilifu, tunaweza kufanya vizuri katika michezo na uchumi wa taifa kwa ujumla”.
Aidha, Waziri Mkuu ameziagiza Mamlaka zote zinazosimamia na kuendesha michezo na sanaa katika shule ziwajibike kikamilifu kuhakikisha mashindano UMISSETA na UMITASHUMTA yanakuwa endelevu “tafuteni mbinu mbadala za kupata washirika zaidi wa kugharamia michezo hii”.
Pia, Waziri Mkuu aliwaasa vijana kujiepusha na vitendo vitakavyokwamisha ndoto zao za kufanikiwa katika masomo na michezo kama vile matumizi ya madawa ya kulevya, uvivu na utoro shuleni.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema kuwa wataendelea kusimamia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kusimamia michezo ili iwe chimbuko la kuvumbua vipaji vitakavyozitumikia timu zetu za taifa na kuchezo katika ngazi za kimataifa.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI David Silinde amesema kuwa michezo hii ya UMITASHUMTA na UMISSETA itakuwa na manufaa na tija kwa taifa letu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.