WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupambana na Dawa za kulevya ambayo kitaifa yatafanyika Mkoani Dodoma.
Katika wiki ya maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zitafanyika katika viwanja vya Nyerere Square ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi ya namna ya kuepuka dawa hizo ambazo huchangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya watu wengi hususani vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Mkuu wa Mkoa Antony Mtaka amesema ni muhimu wakazi wa Dodoma wakatumia fursa hiyo kujitokeza kupata elimu ili kuepuka kujiingiza kwenye matumizi ya dawa hizo.
‘’Wakazi wa Dodoma wanakaribishwa kushiriki kupata elimu, lakini pia ni fursa kwa vijana kujitokeza kupata elimu kwani wengi wamekatisha ndoto zao kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, watakuwepo pia wahanga wa matumizi ya dawa na wataeleza yale waliyoyapitia katika safari yao’’ amesema Mtaka.
Wakati huo huo, Mtaka amewaomba Waandishi wa Habari kutumia taaluma zao kuelimisha jamii kuhusu wiki ya maadhimisho ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ikiwemo madhara yake.
‘’nawaomba muweke uzito wa jambo hili ili tuwe na Dodoma salama hayo yakose nafasi, tutashirikiana na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya kuondoa tatizo hilo’’ amefafanua zaidi Mtaka.
Kwa upande wa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gellard Kusaya amesema dawa za kulevya zisipodhibitiwa nguvu kazi ya Taifa itapotea hasa vijana .
‘’Dawa hizi zinamadhara ndiyo maana zinadhibitiwa, tusipodhibiti tutakosa nguvu kazi kwa vijana, tunataka kuwa na Tanzania huru isiyotumia dawa za kulevya’’ amesema Kusaya.
Katika udhibiti wa Dawa za kulevya Kusaya amesema udhibiti umekuwa mkubwa kwani tangu ameingia madarakani kwa mara ya kwanza wamekamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kilo 859.36.
‘’hali inaonesha udhibiti wetu umekuwa mkubwa, kwa mara ya kwanza tangu Tanzania kupata uhuru tumekamata kiasi kikubwa cha dawa hizo ilikuwa ni mwezi wa nne, ni kiwango kikubwa sana cha dawa kukamatwa kwa mara moja’’, amesema Kusaya
Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za kulevya huadhimishwa June 26 ya kila mwaka, kwa mwaka huu yanakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo ‘’Tuelimishane juu ya tatizo la Dawa za kulevya, Kuokoa Maisha’’
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.