WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa nchini waakisi utashi wa kisiasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.
“’Utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mfumo wa utoaji wa Haki Jinai lazima udhihirike kwenu ninyi viongozi mlio karibu na wananchi. Hata hivyo, utashi huo hauwezi kudhihirika kwenu iwapo hamtakuwa na nia ya dhati ya kubadilika na kisha kuongoza mabadiliko kwenye maeneo mnayomwakilisha Mheshimiwa Rais wetu na hususan katika kuhudumia wananchi,” amesema.
Ametoa wito huo wakati akifungua warsha ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya kuwajengea uelewa kuhusu maboresho kwenye mfumo wa Haki Jinai na utoaji wa haki nchini kwenye ukumbi wa mikutano wa Tume Huru ya Uchaguzi, uliopo Njedengwa, nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Amesema sambamba na suala la utashi, ni lazima viongozi na watendaji wa Serikali wawe na uelewa wa kutosha ili waweze kuyasimamia na kuyatekeleza mapendekezo hayo.
Amesema malalamiko ya wananchi katika masuala kadhaa ndiyo yaliyoweka msukumo kwa Mheshimiwa Rais kuunda Tume ya Haki Jinai na kuyakubali mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo na hatimaye kuigeuza kuwa Kamati ya kuandaa mikakati utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.
“Hivyo basi, kwa kuwa ninyi ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais katika maeneo yenu ya utawala, ni wajibu wenu kuhakikisha kuwa azma ya Mheshimiwa Rais inatimia kwa kusimamia na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai,” amesisitiza.
Akitaja masuala yaliyolalamikiwa na wananchi, Waziri Mkuu amesema utungaji wa baadhi ya sheria ndogo katika mamlaka zao ambazo aghalabu hukinzana na sheria mama. “Mfano ni tozo zinazoanzishwa na halmashauri kama vile ushuru wa mabango, kodi za maegesho na usimamizi wa matumizi ya maeneo ya barabara zinasababisha mkanganyiko kwa wananchi kwa kuwajibishwa na chombo zaidi ya kimoja,” amesema.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.