WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako amefunga maonesho ya pili ya elimu na mafunzo ya ufundi, na kuwashukuru Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi kwa kutambua mchango wa sekta binafsi ikiwemo kushiriki katika maonesho hayo.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati akifunga maonesho hayo leo Juni 2, 2021 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma ambapo maonesho hayo yamefanyika kwa siku saba. Waziri huyo alisema maonesha hayo yalitanguliwa na kongamano lililofanyika terehe 27 Mei, 2021 ambapo jumla ya washiriki 146 walihudhuria.
“Napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa dhati washiriki wote wa maonesho ya pili ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi ambayo yana kaulimbiu ya kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kukuza ujuzi wa maendeleo ya uchumi wa viwanda”, alisema Ndalichako.
Waziri huyo wa Elimu alisema kuwa, ana uhakika kuwa ushirikiano uliooneshwa na ujuzi utaendelea kukuzwa, kwani maonesho hayo yatakuwa ni endelevu kwa miaka inayokuja. Pia alisema elimu ya ufundi ni nyenzo kubwa ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa haraka kwa sababu mafunzo ya ufundi yanampatia na kumuandaa mhitimu kuwa mbunifu zaidi.
‘’Elimu ya ufundi inahitajika sana katika soko la ajira kwa sababu inaleta maendeleo na matokeo ya haraka endapo itatolewa kwa viwango vinavyotakiwa’’ alisema Ndalichako.
Aidha, alisema katika maonesho hayo vyuo na tasisi za ufundi zimepata fursa ya kueleza na kuonesha kwa wadau kile wanachokifanya katika vyuo vyao au katika taasisi zao. “Ni matarajio yangu kwamba, maonesho haya yameamsha ari mpya ya ushirikiano baina ya wadau na watoaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi na kwamba ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali ni muhimu katika kuboresha utoaji wa elimu ya kati na ya juu nchini” alisema Ndalichako.
Vile vile ametoa pongezi kwa vyombo vya habari kwa kushiriki kwenye maonesho kwa kipindi chote na kuonesha ushirikiano mkubwa katika kuyatangaza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.