WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu, amezitaka sekretarieti za Mikoa yote hapa nchini kuhakikisha zinatimiza wajibu wake kwa weredi na kuongeza kasi katika kushauri maswala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Mikoa hiyo hasa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Waziri Ummy ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akizungumza viongozi na watumishi wa ngazi zote katika Mkoa wa Dodoma, alipokutana nao kuweka mikakati ya pamoja katika kuendesha Wizara hiyo, amesema sekretarieti za Mikoa ndizo zenye wajibu wa kumshauri Mkuu wa Mkoa juu ya maswala mbalimbali yanayohusu Mkoa husika.
Amewataka kujenga utaratibu wa kuzitembelea halmashauri zote za Mikoa na kwenda kufanya tathmini ya mipango na utekelezaji wake kwa kila robo ya mwaka ili kubaini vikwazo na kuzitatua kwa wakati ili kufikia malengo waliyojiwekea katika halmashauri husika.
“Kila robo ya mwaka mkae kwa pamoja aidha muwaite kwenu au muende kwao mkakae kwa pamoja muangalie mipango yenu imefikia wapi, walitakiwa wakusanye kiasi flani kwanini hawajafika lengo, kuna fedha imekusanywa kwanini haijaingizwa benki, kuna mradi hawajaomba fedha kwanini” amesema Waziri Ummy.
Kuhusu ripoti ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali CAG Waziri Ummy amewataka kuwabainisha wote waliohusika katika ubadhilifu, waliosababisha au uzembe uliofanywa hadi kupelekea halmashauri kupata hati chafu au hati yenye mashaka na kuwachukulia hatua stahiki.
Katika hatua nyingine amewataka kuongeza kasi ya utatuzi wa kero za wananchi kwani amesema kuna malalamiko mengi sana katika maeneo mbalimbali hasa katika maswala ya ardhi huku akiwataka kujenga tabia ya kuwasikiliza wananchi kero zao na sio kuwa wao ndio wawewazungumzaji pekee.
“nilikuwa nazungumza na wakuu wa Mikoa wa zamani wanasema wao walikuwa wakienda hadi ngazi za chini kabisa, lakini sasa hivi huo utaratibu umepungua, nataka wakuu wa Mikoa muende hadi ngazi za kata mkae huko msikilize kero za wananchi na wakuu wa Wilaya waende hadi ngazi za Kijiji” amesema.
Amepongeza juhudi kubwa zilizofanyika katika Mkoa wa Dodoma katika utendaji kazi na utekelezaji wa miradi na kuwataka kuongeza kasi, amepongeza katika sekta ya elimu kwa kuongeza ufaulu kwa shule za msingi kutoka ufaulu wa asilimia 53 hadi kufikia asilimia 76 na sekondari kutoka asilimia 64 hadi kufikia asilimia 87.
Amepongeza juhudi zilizofanyika hasa katika miradi ya elimu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari, sambamba kwenye sekta ya afya na miondombinu yake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.