WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amefanya ziara katika hospitali ya Uhuru iliyopo Wilaya ya Chamwino kukagua Maendeleo yake na kuagiza kuanza ujenzi wa majengo ya awamu ya pili ili kupanua zaidi wigo wa upatikanaji wa huduma za afya.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kukagua maendeleo katika hospital hiyo Waziri Ummy amesema mara baada ya baadhi ya huduma kuanza kutolewa sasa waanze mchakato wa ujenzi wa majengo ya awamu ya pili yatakayojumuisha na wodi za kulaza wagonjwa.
“Sasa hapa tumeona kazi kubwa imefanyika zimebaki kazi ndogo ndogo ili ujenzi wa awamu ya kwanza ukamilike, naona na huduma zinatolewa, sasa tuanze mchakato wa ujenzi wa awamu ya pili tujenge mawodi hapa ni barabarani lazima tupanue zaidi huduma” amesema Waziri Ummy.
Amesema hospital hiyo ni kubwa sana na inahudumia mpaka Mikoa na Wilaya za karibu hivyo ni muhimu ujenzi wa awamu ya pili ukamilike kwa wakati kuwapunguzia wananchi kupata huduma mbali ambapo kwa sasa baadhi ya huduma wanafuata hospitali ya rufaa Dodoma na Benjamini Mkapa.
Amesema Serikali ya sasa itayaendeleza mambo yote yaliyoanzishwa na hayati Dkt Magufuli ambapo sasa watatoa kiasi cha shilingi bilioni 1.7 zinazohitajika ili kukamilisha kazi ndogo ndogo zilizobaki kukamilisha awamu ya kwanza ya and ujenzi.
Amewakata watumishi katika hospitali hiyo kufanya kazi kwa weredi na kufuata maadili ya kazi yao wanapotoa huduma kwa wananchi na kutoa kauli nzuri kwa wagonjwa wanapowahudumia.
Pia ametaka watumishi katika hospitali hiyo na watumishi wengine kuwahamasisha wananchi kujiunga katika mfuko wa bima ya afya kuwapunguzia gharama za matibabu wanapougua.
“Tuwahamasishe wananchi wajiunge na mfuko wa bima ya afya, ukiangalia kuna wagonjwa kujiandikisha tu anatoa elfu kumi na tano (15,000) wakati angekuwa na bima hata ile ya elfu thelathini(30,000) asingelipa hiyo elf kumi na tano” amesema.
Aidha amewatoa hofu watumishi wanaofanyakazi za kujitolea katika hospitali kuwa serikali itawapa kipaumbele katika katika ajira zitakazotolewa huku akitaka kuwe na kanzi data ya watumishi wanaojitolea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Naagiza Waganga wakuu wa Wilaya mkasimamie hilo na kwenye data base (kanzi data) watumishi hao waainishwe kaanza kujitolea lini, isije kuwa kesho wakafurika watu wa kujitolea baada ya kusikia watapewa kipaumbele kwenye ajira” amesema.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambaye alikuwa msimamizi wa ujenzi Athumani Masasi amesema ujenzi ulianza rasmi Novemba 26, 2019, kwa kutumia force akaunti kwa kutumia mkandarasi SUMA JKT na mpaka sasa Ujenzi wake umefikia asilimia 98.2.
Amesema Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje tangu Desemba 21, 2020 na inawatumishi 52 kati ya watumishi 117 wanaohitajika, na mpaka sasa imehudumia wagonjwa 3,154, na tayari imekusanya zaidi ya milioni 33.
Ujenzi wa hospital ya Uhuru ni matokeo ya matokeo ya kuahilishwa kwa sherehe za uhuru mwaka 2018 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Dkt Magufuli na kuagiza fedha hizo ziende katika ujenzi wa Hospitali hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.