Na. Sifa Stanley, DODOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi ambaye anasimamia haki za binadamu na utawala bora.
Pongezi hizo alizitoa alipokuwa akihutubia katika kilele cha maadhimisho na maonesho ya miaka 20 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yaliyofanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma.
Waziri huyo alisema kuwa Rais amekuwa akiongoza nchi kwa kuzingatia haki za wananchi wake na kuzingatia utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Wenzetu wa Tume wameandaa zawadi mahususi kwaajili ya Rais wetu, mimi kama Waziri wa Katiba na Sheria nafahamu kwa jinsi gani amepigania watu wa Tanzania waweze kupata haki za kiraia, haki za kisiasa, haki za kiuchumi, haki za kiutamaduni pamoja na haki za kijamii. Tunabahati sana kuwa na Rais ambae anazingatia haki za binadamu na hii inatokana na ukweli kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 8 ibara ndogo ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema wazi kwamba nchi hii ni nchi ya kidemokrasia na yenye kujali misingi ya haki za binadamu kwahiyo haya ambayo Rais anayafanya na Tume inayafanya ni utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Dkt. Ndumbaro.
Aidha, Waziri huyo hakuishia kumpongeza Rais lakini pia aliipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kuendelea kusimamia masuala ya haki za binadamu na wadau mbalimbali wanaoshirikiana na Tume hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Tume katika kutekeleza majukumu yake.
“Tume ya Haki za Binadamu inafanya vizuri na inatoa mchango mkubwa sana katika kusimamia masuala ya haki hapa nchini nawapongeza kwa hilo, lakini pia nichukue nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa wadau mbalimbali ambao wanaiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake hivyo, kuleta maendeleo ya nchi. Wadau namba moja wako hapa ni waheshimiwa wabunge wanaounda kamati ya bunge ya Katiba na Sheria waheshimiwa hongereni sana, bajeti mnayoipitisha kwa Tume ni msaada mkubwa na mnaifanya Tume itekeleze majukumu yake mbalimbali lakini pia na Taasisi nyingine za kimataifa zinaisaidia Tume kutekeleza majukumu yake ninawashukuru sana” alisema Dkt. Ndumbaro.
Maadhimisho ya miaka 20 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa mwaka huu yalianza rasmi tarehe 09/09/2022 na kuhitimishwa tarehe 15/09/2022.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.