Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa ujenzi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kusogeza huduma kwa wananchi na kuongeza mapato.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Dodoma, Zuberi White alipokuwa akifungua Mkutano wa mwaka wa ALAT Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma mwishoni mwa wiki.
White alisema kuwa walitembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuridhishwa na utekelezaji wake. “Tumeona wenzetu wanavyotekeleza mradi wa ujenzi wa hoteli ya Dodoma City, ujenzi wa soko la wazi la Machinga, ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe, ujenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza, ujenzi wa shule ya sekondari Hombolo Makulu na ujenzi wa jengo la kitega uchumi Mtumba, kwa kweli wenzetu hawa wapo vizuri na wamejipanga sawasawa” alisema White.
Alisema kuwa miradi hiyo ni mizuri. Pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi, miradi hiyo itaongeza mapato ya halmashauri, alisema.
Mkutano wa mwaka wa ALAT Mkoa wa Dodoma ulifanyika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitanguliwa na ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini hapo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.