Na. Shaban Ally na Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imefungua ukurasa wa ushirikiano na Baraza la Mji wa Wete kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba ili kuchochea maendeleo ya wananchi wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago alipokuwa akiwakaribisha Madiwani kutoka Baraza la Mji wa Wete, Pemba waliofanya ziara ya kikazi ya siku mbili kutembelea jiji hilo.
Chibago aliwakaribisha na kusema kuwa watapata fursa ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyopo katika Halmashauri yake. Aliwaomba wageni hao kuanzisha uhusiano wenye lengo la kuchochea maendeleo katika maeneo yao pamoja na kudumisha umoja na mshikamano. "Niwaombe ndugu madiwani wenzangu kutoka Wete kwa pamoja tuanzishe ukurasa mpya wa uhusiano kwa lengo la kuchochea maendeleo ya wananchi wetu" alisema Chibago.
Naibu Meya aliwashukuru wageni hao kwa uamuzi wao wa kulitembelea Jiji la Dodoma na kuuita kuwa ni uamuzi sahihi. “Leo nimepata furaha baada ya kuona nimepata ugeni wa madiwani kutoka Wete, wenye lengo la kutaka kujifunza kwa kile kilichofanyika. Hivyo, basi tunashukuru kwa ujio wenu na mjisikie mko nyumbani" alisema Chibago.
Kwa upande wake Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa jiji hilo limeweka nguvu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kukusanya mapato kwa wingi kupitia miradi hiyo. “Kupitia kitega uchumi chetu cha hoteli tunategemea kwa mwaka kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 1.3" alisema Kaunda.
Kaunda alisema kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa kufikia malengo yake kwa kufanya kazi kwa kushirikiana. “Ushirikiano mzuri baina ya viongozi wa halmashauri na wataalam ndiyo msingi wa mafanikio haya tunayoyapata. Nichukue nafasi hii kuwashauri waheshimiwa madiwani kuwa mnapopanga mikakati ya kuleta maendeleo ni vizuri mkazingatia Ilani ya uchaguzi ya chama na kushirikisha wataalam wa maendeleo katika maeneo yenu” alisema Kaunda.
Nae Katibu wa madiwani wa Baraza la Mji wa Wete, Hamadi Ali alieleza kuwa amejifunza kupitia miradi ya maendeleo iliyofanyika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na wao kama viongozi watachukua hatua za utekelezaji watakaporudi katika maeneo yao. “Kiukweli ziara yetu hii ya kuja hapa Dodoma imetufundisha ni kwa kiasi gani tunaweza kubuni njia mpya za kuongeza mapato Katika Halmashauri zetu. Hivyo, na sisi tukirudi Pemba tutakaa chini na Baraza la Madiwani kuweza kutafuta njia mpya za kuongeza mapato” alisema Ali.
Kwa upande mwingine, Diwani wa kuteuliwa wa Wete, Aisha Hamadi alitoa wito kwa viongozi wenzake wa halmashauri nyingine kutembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kujifunza juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao. “Wito wangu kwa viongozi wenzangu ni kwamba waje kujifunza vitu mbalimbali vya kimaendeleo kwa kuwa kuna miradi mikubwa ya maendeleo imefanyika kama vile mradi wa soko la wazi la Machinga” alisema Aisha.
Diwani huyo alitoa pongezi zake za dhati kwa madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa jitihada zao za kuifanya Dodoma kuwa na hadhi ya juu inayostahili.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.