WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH) ni miongoni mwa Wizara na taasisi nyingine za Kiserikali ambazo zimepongezwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na ushirikiano katika kufanikisha Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Hafla rasmi ya kuzindua matokeo ya awali ya Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imehudhuriwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma tarehe 31 Oktoba 2022.
Akizungumza jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi nyingine zilifanya Operesheni ya Anwani za Makazi vizuri kiasi kwamba ni sehemu ya mafanikio ya sensa ya mwaka huu 2022. WHMTH ilisimamia utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi iliyofanyika kuanzia mwezi Februari 2022.
"Nazindua matokeo yanayoonesha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina idadi ya watu milioni 61,741,120" alisema Rais Samia Suluhu Hassan. Idadi hiyo ni ongezeko kutoka idadi ya watu milioni 44.9 ya Sensa iliyofanyika mwaka 2012.
Rais Samia alisema kati ya watu milioni 61.7, Tanzania Bara inachangia idadi ya watu milioni 59,851,357 wakati Zanzibar ina watu milioni 1,876,773.
Sensa ya Taifa ya mwaka 2022 ilifanyika kwa njia ya kidijiti, mfumo wa kisasa wa kukusanya takwimu ambao umepongezwa na jumuiya za kimataifa likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNPF).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.