HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma yaadhimisha wiki ya maziwa kwa kugawa Ng’ombe 12 kwa vikundi vitano vya wajawasiliamali, ng'ombe hao wamenunuliwa kupitia fedha za mapato yake ya ndani kwa lengo la kuwainua kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe katika hafla fupi ya kukabidhi Ng’ombe 12 kwa vikundi vitano tukio lililofanyika katika viunga vya ofisi za Jiji zilizo karibu na eneo la Sabasaba jijini Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa Halmashauri inakabidhi Ng’ombe hao kwa lengo wa kuwasaidia wananchi kukua kiuchumi. “Tukio hili kwa Halmashauri ya Jiji linakwenda sambamba na wiki ya unywaji maziwa ambayo kilele chake ni leo. Hapa Jiji la Dodoma, sisi ni washiriki kwa vitendo katika hili” alisema Prof. Mwamfupe.
Akiongelea tukio la kukabidhi Ng’ombe hao alisema kuwa ni moyo wa huduma kwa wananchi. “Tunakabidhi Ng’ombe hawa 12 hapa, si kuwa ni ishara ya kuonesha utajiri wa Halamshauri, bali ni moyo wa kujitolea wa Halmashauri kuwahudumia wananchi wake” alisema Prof. Mwamfupe.
Mtahiki Meya huyo aliwataka wanavikundi waliopata Ng’ombe hao kuwatunza na kuwahudumia kwa kufuata maelekezo ya wataalam. Aidha, aliwataka wataalam wa mifugo katika kata kutoa ushauri wa kitaalam kwa wanavikundi hao ili wafuge kwa manufaa. “Ole wako mtaalam wetu wa mifugo kwenye kata tusikie ng’ombe amekufa sababu hukwenda kumhudumia” alionya Prof. Mwamfupe.
Akitoa maelezo mafupi ya hali ya ukopeshaji vikundi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alisema kuwa vikundi vitano vinapatiwa Ng’ombe wa maziwa kutoka mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. “Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, vikundi hivi ni baadhi tu ya vikundi ambavyo tumetoa mikopo kwa awamu hii. Mwaka huu wa fedha Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumetoa shilingi bilioni 1.7 kwa vikundi mbalimbali. Vikundi hivyo vimenufaika kwa kutekeleza miradi ya aina mbalimbali. Vikundi hivi vitano viliamua kufanya shughuli ya ufugaji” alisema Nabalan’anya.
Akiongelea upatikanaji wa Ng’ombe hao, Nabalang’anya alisema kuwa Idara yake kwa kushirikiana na Idara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi walihakikisha kuwa fedha zinazoingizwa katika akaunti za vikundi hivyo zinaunganishwa pamoja na kuagiza Ng’ombe. “Ng’ombe hawa wametoka Arusha na wanathamani ya shilingi milioni 24. Ni Ng’ombe 12, kwa gharama ya manunuzi mpaka kuwafikisha hapa kila Ng’ombe amegharimu shilingi milioni mbili. Lakini jumla ya fedha ambazo vikundi hivi vimenufaika ni shilingi milioni 44, kwa hiyo bado kila kikundi kina kiasi cha fedha kwa ajili ya chakula, dawa na chanjo” alisema Nabalang’anya.
Kwa upande Kaimu Afisa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi Jiji la Dodoma, Gratian Mwesiga alisema kuwa Ng’ombe wanaogawiwa ni mitamba yenye mimba kati ya miezi sita hadi saba. “Umri wao ni kati ya miezi 18-22. Ng’ombe anauwezo wa kuzaa ndama 10 kwa maana maisha yake ya kuishi ni miaka 10. Hivyo, kila mwaka kama mambo yataenda vizuri atakuwa anazaa ndama mmoja mmoja” alisema Mwesiga. Aidha, alisema kuwa matarajio ya Halmashauri ni vikundi hivyo vifuge ng’ombe hao kwa miaka 10. Vilevile, aliwataka wanavikundi hao kufuata ushauri wa wataalam wa mifugo ili kuweza kufuga kwa tija.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana Sharifa Nabalang'anya akifafanua jinsi mikopo ya asilimia 10 kutoka katika mapato ya ndani ya Jiji la Dodoma ilivyowanufaisha wananchi wa Jiji la Dodoma.
Kaimu Afisa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi Jiji la Dodoma, Gratian Mwesiga akiongelea ubora na faida inayotarajiwa kutoka kwa ng'ombe ambao Jiji la Dodoma limefanikisha upatikanaji wao ili kuwa chachu ya maendeleo ya wananchi wa jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.