HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imejipanga kutoa elimu ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa wananchi kupitia vituo vya afya na redio za ndani ya Jiji la Dodoma katika mkakati wake wa kukabiliana na tatizo la lishe.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Eva Juma alipokuwa akiongelea maandalizi ya Jiji hilo kuelekea wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama inayoanza tarehe 1-7 Agosti, 2020.
Juma amesema kuwa katika wiki hiyo kila kituo cha Afya chenye huduma ya mama na mtoto kitatoa elimu ya umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama miezi sita ya mwanzo mpaka miaka miwili. Alisema kuwa katika wiki hiyo suala la ulishaji watoto wadogo kuanzia miezi sita mpaka miaka miwili litapewa kipaumbele.
Afisa Lishe huyo amesema kuwa kwa wananchi walio katika ngazi ya kata na jamii, watoa huduma ngazi ya jamii watatumika kuihamasisha jamii kuhusiana na unyonyeshaji maziwa ya mama. Elimu hiyo inaendelea kutolewa katika vituo vya redio vilivyopo ndani ya Jiji la Dodoma na mitandao ya kijamii ili kuhakikisha inawafikia wananchi wengi.
Uzinduzi wa wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama utafanyika tarehe 1 Agosti, 2020 jijini Dodoma ukiongozwa na kaulimbiu isemayo “tuwawezeshe wanawake kunyonyesha kwa afya bora na ulinzi wa mazingira”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.