WILAYA ya Dodoma imepanua kituo cha Afya Mkonze kwa kuongeza majengo matano kwa lengo la kupanua wigo wa utoaji huduma kwa wananchi ambazo hazikuwepo awali.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akisoma risala ya utii kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Dodoma kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya na kusema kuwa Wilaya kwa kushirikiana na serikali kuu imepanua kituo cha Afya Mkonze kwa kuongeza majengo matano. Aliyataja majengo hayo kuwa ni jengo la maabara, huduma za uzazi, jengo la upasuaji, nyumba ya mtumishi na jengo la kuifadhia maiti yenye thamani ya shilingi 687,826,442. “kiasi cha shilingi 400,000,00 kimetolewa na serikali kuu na shilingi 287,826,442 ni mchango wa Halmashauri ya Jiji. Ujenzi huu ukikamilika utasaidia kupanua wigo wa utoaji huduma ambazo awali hazikuwepo kama huduma za upasuaji, nyumba ya mganga mkuu na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa mwananchi wa Wilaya ya Dodoma” alisema Kunambi.
Kwa upande wa kituo cha Afya Makole, alisema kuwa Wilaya kwa kushirikiana na serikali kuu imefanikiwa kupanua kituo hicho kwa kuongeza majengo matano ambayo ni jengo la maabara, jengo la huduma ya mama na mtoto, jengo la upasuaji, nyumba ya mtumishi na jengo la kuifadhia maiti yenye thamani ya shilingi 572,688,056. Kiasi cha shilingi 500,000,000 kimetolewa na serikali kuu na shilingi 72,688,056 zilitolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, aliongeza. “Ujenzi huu umekamilika na kituo kinatoa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Dodoma takribani watu 320 kwa siku” alisema Kunambi.
Akiongelea dhamira ya Wilaya kufikia uchumi wa viwanda, alisema kuwa Wilaya imekua ikihamasisha na kushauri wananchi kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali mfano wa kikundi cha umoja wa wakulima wa zabibu na masoko Mpunguzi (UWAZAMAMU). “Kikundi hiki kilianza kama chama cha msingi cha ushirika cha wakulima wa zabibu kwa namba ya usajili SR 535 kikiwa na wanachama 50 hadi tarehe 30 Julai, 2019 kikundi kilikuwa na kiwanda cha kuchakata mchuzi wa zabibu na wanachama waliongezeka na kufikia wanachama 196. Mradi huu umegharimu jumla ya shilingi 112,000,000. Fedha hizo ni michango ya wanakikundi, wadau wa maendeleo – shirika la Lutheran World Relief la Marekani na serikali kuu kupitia mradi wake wa TSCP” alisema Kunambi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa punguzo la kodi ya mchuzi wa zabibu imepelekea bei ya mchuzi kuongezeka kutoka shilingi 1,200 hadi shilingi 1,730 kwa lita moja. Kutokana na ongezeko hilo, kiwanda kitachangia zaidi katika kukuza uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla, aliongeza.
Akiongelea maendeleo ya sekta ya maji, alisema ”katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya Maji pamoja na utunzaji wa vyanzo vyake kama ujumbe wa Mwenge wa mwaka 2019 unavyosema ‘Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchanguzi wa Serikali za mitaa’ Wilaya imefanikiwa kutoa mafunzo na kusajili Jumuiya za watumiaji maji 22 kama vyombo halali vya usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji katika vijiji/mitaa 18” alisema Kunambi.
Wilaya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekamilisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya miradi ya maji mitatu kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza Wilaya ilikamilisha ujenzi wa miundombinu katika vijiji/mitaa tisa ambapo vituo vya kutekea maji 158 vilijengwa vyenye vitekeo 316. “Jumla ya watu 53,471 wananufaika na mradi huo. Awamu ya pili Wilaya ilikamilisha ukarabati wa miradi mikubwa miwili yenye jumla ya shilingi 212,000,000 iliyopo katika kata za (Mbalawala-Chihikwi shilingi 90,000,000 na Zuzu shilingi 122,000,000)” alisema. Aidha, awamu ya tatu Wilaya inaendelea na ujenzi wa mradi wa maji katika kata ya Hombolo Bwawani ambao umetengewa shilingi 500,000,000 na ukikamilika utahudumia watu wapatao 10,567.
Mwenge wa Uhuru umemaliza mbio zake tarehe 15 Agosti, 2019 asubuhi wilayani Dodoma na kukabidhiwa Wilaya ya Chemba.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.