Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapenzi yake kwa watanzania kuruhusu chanjo ya UVIKO-19 kupokelewa nchini na kuongoza zoezi la uchanjaji ili kujikinga.
Shukrani hizo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na wataalam wa afya na watu waliojitokeza kuchanjwa katika uzinduzi wa chanjo ya UVIKO-19 Wilaya ya Dodoma, tukio lililofanyika katika Kituo cha Afya Makole jijini Dodoma.
Shekimweri alisema “nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutujalia afya njema. Pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa nia yake njema na mapenzi kwa nchi yake alipokubali kupokea dozi 1,000,000 za chanjo ya UVIKO-19”.
Akiongelea usalama wa chanjo hiyo, alisema kuwa chanjo ni salama. Mheshimiwa Rais amechanja tayari. “Napenda kuwatoa hofu wale wote wenye hofu, mimi mwenyewe nimechanja jana, na leo nipo salama na kazi iendelee. Tutafute taarifa sahihi toka kwa wataalam wa afya siyo kwenye mitandao ya kijamii inayopotosha baadhi ya taarifa” alisema Shekimweri.
Kuhusu mwitikio wa watu kujitokeza kuchanja, alisema kuwa mwitikio ni mkubwa. “Jana watu waliojitokeza kuchanja ni 1,135 kwa Wilaya ya Dodoma wakati makadilio ilikuwa kuchanja watu 600. Kwa kituo cha Afya Makole jana walijitokeza kuchanja watu 194 kati ya makadilio ya kuchanja watu 200” alisema Shekimweri.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuzindua zoezi la uchanjaji chanjo ya UVIKO-19, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa Wilaya ya Dodoma ina jumla ya vituo saba. Kituo cha Afya Makole kimejipanga kutoa chanjo ya UVIKO-19 na kimetenga maeneo mawili ya kutolea chanjo hiyo. Alisema kuwa maeneo yataongezwa kutegemea na wingi wa watu wanakavyojitokeza kuchanjwa.
Akiongelea usalama wa chanjo hiyo, Mganga mkuu huyo alisema kuwa chanjo hiyo ni salama. “Nichukue nafasi hii kuwatoa hofu wananchi. Chanjo hii ni salama na chanjo ni kinga. Tutumie nafasi hii kuhakikisha tunachanja” alisema Dkt. Method.
Nae Afisa Habari wa timu ya Dodoma Jiji FC, Moses Mpunga aliyekuwa mtu wa pili kuchanja baada ya uzinduzi huo, alisema kuwa chanjo hiyo ni muhimu. “Kwanza naipenda afya yangu, lakini pia napenda kuwalinda walionizunguka. Mimi nikichanjwa nitakuwa nipo mbali zaidi ya kupata virusi vya UVIKO-19 kwa sababu mwili utakuwa unakinga. Na hata nikipata madhara yake hayatakuwa makubwa” alisema Mpunga.
Aliwataka wakazi wa Wilaya ya Dodoma kuachana na Habari potofu dhidi ya chanjo hiyo. “Rai yangu kwa wanadodoma wanatakiwa kuachana na hadithi za kufikirika sababu maisha ni ya mtu binafsi. Asilimia kubwa ya watu wanaoshawishi wengine wasichanje wameshachanjwa” alisema Mpunga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.