Na. Sifa Stanley, DODOMA
AFISA kilimo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Agness Woisso ametoa wito kwa wananchi kutembelea maonesho ya wakulima na wafugaji Nanenane ili wajifunze mbinu za kisasa za kilimo.
Wito huo aliutoa katika viwanja vya Nanenane, Nzuguni alipokuwa akitoa maelezo ya namna halmashauri ilivyojipanga kuhakikisha kuwa wakulima na wananchi wananufaika na maonesho hayo, tofauti na miaka iliyopita.
“Tunawakaribisha wakulima waje kwasababu teknolojia iliyopo ni nzuri na ya kisasa. Pia kuna wakulima ambao watakuwa wanatoa maelezo na elimu kwa wakulima wengine kwasababu kuna wakulima wakipewa maelezo na afisa kilimo wanakuwa kama vile hawaamini, lakini wakielekezwa na mkulima mwenzao ni vizuri zaidi, kwa hiyo kuna wakulima tumewaalika ili watoe ushuhuda” alisema Woisso.
Aidha, aliwashauri wananchi kuanzisha kilimo cha bustani nyumbani kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ambayo itawasaidia kulima mbogamboga nyingi katika eneo dogo. Alisema kuwa teknolojia hiyo itawasaidia kujikwamua kiuchumi.
“Katika banda letu tumeandaa teknolojia mbalimbali za kilimo kwaajili ya kuwafundisha wakulima. Kuna kilimo cha bustani za mbogamboga zimelimwa katika vipando vyetu. Bustani za nyumbani kama tunavyojua jiji letu limepimwa na maeneo ya kilimo yamepungua, tunawahamasisha wakulima walime bustani za nyumbani kwa kutumia viroba ili waweze kujikwamua kiuchumi” alisema Woisso.
Akieleza namna alivyonufaika na maonesho hayo Emmi Alex, mkazi wa Meriwa alisema kuwa maonesho hayo yamempa fursa yakujifunza masuala mbalimbali ya kilimo ambayo ni muhimu kwa wananchi wote kujifunza na si wakulima peke yao.
“Nimefurahi kufika katika maonesho haya ya Nanenane kwasababu nimeona mambo mengi mazuri. Pia nimejifunza mambo ambayo sio wakulima pekee wanapaswa kujifunza hata mtu binafsi anaweza kujifunza kama vile kilimo cha bustani mtu akanufaika na kilimo” alieleza Alex.
Maonesho ya Nanenane yalianza Agosti 1, 2022 na yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 8, 2022 yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Wekeza katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa maendeleo ya Viwanda”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.