Na. Sifa Stanley, DODOMA
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali yametakiwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na mashirika hayo katika kuwahudumia wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asha Vuai alipokuwa akifunga kikao cha wadau wa afua za afya ya uzazi na maendeleo ya vijana kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Vuai alisema kuwa ni muhimu mashirika yasiyo ya kiserikali yakafanya kazi kwa ushirikiano. Ushirikiano huo unaweza kuwa baina ya mashirika hayo na serikali ili kufikia malengo yaliyowekwa, aliongeza. Aidha, aliahidi kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo ili kuyasaidia kutekeleza majukumu yao.
“Nitatoa ushirikiano pale utakapohitajika. Nipo ofisini kwangu, karibuni mkiwa na uhitaji. Tunajenga nyumba moja yanini kugombania fito? Tushirikiane, napata matumaini kupitia kwenu, maendeleo ya vijana yatapatikana” alisema Vuai.
Nae Afisa Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mufungo Manyama alipokuwa akiongea na wadau wa afua za afya ya uzazi na maendeleo ya vijana alisisitiza wadau kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano ili kunufaisha jamii na taifa “ninachotaka wadau tufanye kazi kwa pamoja. Waswahili wanasema ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako, lakini ukitaka kufika haraka nenda peke yako. Kwahiyo, sisi twende pamoja” alisema Manyama.
Kwa upande wake, Afisa Uraghibishi wa Mradi wa Shirika la Dodoma Youth Development Organization (DOYODO), Hawa Ally alitoa rai kwa washiriki wengine kushirikiana ili waweze kuinufaisha jamii kupitia miradi wanayofanya. “Tuwe tunaungana kwa pamoja kupitia hivi vikao, ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja na kuepuka kurudiarudia mradi mmoja unaofanana kwa mashirika yote ndani ya kata moja” alisema Ally.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.