Dodoma sasa ni jiji na maeneo mengi yamepimwa, na kazi ya upimaji na upangaji mji inaendelea. Kwa hiyo hatuna budi kuhakikisha maeneo ya jiji sasa yanakuwa safi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu wa Jiji la Dodoma Dickson Kimaro aliposhiriki katika kufanya usafi wa kila jumamosi leo kwenye eneo la kihistoria inaposemekana kuwa tembo alizama, na hapo ndipo penye asili ya jina Dodoma lililotokana na neno 'Idodomya' (alizama).
Moja na sifa ya maeneo ambayo yamepimwa ni maeneo hayo kuonekana ni masafi, na kwa hivi sasa taka zote zinatakiwa kukusanywa na kusafirishwa kwenda kwenye dampo moja tu la kisasa lililopo Chidaya.
Ikumbukwe Mkuu wetu wa mkoa alishatoa tamko akihitaji mkoa anaouongoza uwe safi. Tamko hili alilitoa Chigongwe na Jiji la Dodoma limekuwa tukiendelea kulifanyia kazi tamko hilo kwa kila jumamosi kufanya usafi wa mazingira.
Lengo ni kuwafanya wananchi wabadilike tabia, wawe na tabia ya kufanya usafi bila shuruti, wafanye usafi kwa hiari yao bila ulazima wa matangazo kutoka Jiji, polisi jamii, mgambo, au watendaji wa kata na mitaa. Kila mmoja kwenye eneo lake la biashara au kwenye makazi.
Kimaro alikumbusha kauli mbiu ya usafi ni USAFI WA MAZINGIRA MITA TANO kuzunguka maeneo yako. Madhumuni ni kufanya maeneo ya Jiji kwa ujumla wake yawe safi wakati wote.
"Tunahitaji jiji la Dodoma kuwa la mfano kwenye maeneo yote kama tulivyo mfano mzuri kwenye makusanyo ya fedha za vyanzo vya ndani vya mapato yetu. Tunahitaji maeneo yote ya Chigongwe, Nala, Veyula hadi katikati ya Jiji kuwe safi. Hilo linawezekana kama kila mmoja akitimiza wajibu wake, shime viongozi wa kata, mitaa na wananchi tuendelee kulisimamia jambo hili", amesema Kimaro.
Hata hivyo, Kimaro alisisitiza kuwa Jiji litaendelea kufuatilia na kama mtu atavunja sheria basi atachukulia hatua za kisheria ikiwemo kupigwa faini kati ya shilingi hamsini elfu hadi shilingi laki tatu.
Kimaro alikumbusha kuwa Makamu wa Rais mama Samia alizindua kampeni ya "Dodoma ya Kijani". Na kwamba Jiji kwa kushirikiana na TFS wanatarajia kuotesha miche ya miti milioni mbili ili kudhibiti uharibifu wa mazingira unaoendelea. Miche hiyo itasambazwa kwenye maeneo mbalimbali ili watu wapande miti. "...licha ya kupanda mti, tunategemea utakapoupanda mti, uweze pia kutekeleza jukumu la kuutunza ili ukue vizuri" alisisitiza.
Mkuu huyo wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa taka ngumu alisema "Jambo lingine, miti iliopo na ile tutakayoendelea kuipanda tuhakikishe hatuikati hovyo. Hivi sasa kwa taratibu ambazo jiji limeweka ni kwamba hata kama mti umeupanda wewe mwenyewe, bado huruhusiwi kuukata bila kibali kutoka Jiji la Dodoma".
Akifafanua zaidi Kimaro alisema, Jiji la Dodoma limeweka sharti kwenye vibali vya ujenzi kuwa ni lazima kupanda miti isiyopungua mitano katika eneo lako la ujenzi. Miti hiyo itajumuisha miti ya kivuli na miti ya matunda. Kimaro ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma kutokata miti na kuwazuia wote watakaobainika kutaka kukata miti.
Aidha, amekemea watu wanaotumia mifuko la plastiki myeupe ambayo ilikuwa ikitumika kama vifungashio lakini watu wamegeuza matumisi yake na kuifanya kuwa vibebeo. Amesema Waziri mwenye dhamana na Mazingira Mhe. Simbachawene ametoa muda wa wiki mbili tu wenye mifuko waisalimishe na taratibu za kuiangamiza zitafanywa na Jiji.
Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu Dickson Kimaro akiongea na wananchi mara baadha ya kukamilisha zoezi la usafi wa Jumamosi katika kata ya Kikuyu Kusini mahali ambapo inasadikika tembo alizama, na ndipo penye chanzo cha jina la Dodoma (Idodomya - alizama).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.