Na. Dennis Gondwe, Chinangali Park - DODOMA
WAKAZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujitokeza na kujiandikisha katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF Iliyoboreshwa) ili wapate huduma ya matibabu ya afya kwa gharama nafuu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa CHF iliyoboreshwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga alipokuwa akitoa elimu ya umuhimu wa CHF iliyoboreshwa kwa wananchi waliotembelea banda la Afya la halmashauri hiyo katika Bustani ya Mapumziko Chinangali jijini Dodoma kwenye maonesho ya Karibu Dodoma Festival.
Sebyiga alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inashiriki katika Karibu Dodoma Festival kwa lengo la kuhamasisha, kuandikisha na kusajili wanachama kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii. “Natoa wito kwa wananchi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutembelea banda la afya la Halmashauri katika Bustani ya Mapumziko Chinangali ili kujiunga na CHF iliyoboreshwa. Gharama yake ni nafuu sana, shilingi 30,000 kwa kaya moja unapata matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima” alisema Sebyiga.
Akiongelea faida za Mfuko wa Afya ya Jamii, Mratibu huyo alisema kuwa mwanachama anapata huduma bora za afya kwa kipindi cha mwaka mzima. “CHF iliyoboreshwa ina faida nyingi, mwanachama anapata huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu ikiwepo huduma ya upasuaji mkubwa na mdogo. Faida nyingine ni vipimo vya maabara na afya ya mama na mtoto pamoja na huduma za wagonjwa wa kutwa na kulazwa kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Afya” alisema Sebyiga.
Mfuko wa Afya ya Jamii ni mpango muhimu wa hiari ulioanzishwa kwa sheria Na. 1 ya mwaka 2001 wa kaya, familia, kikundi au mtu binafsi kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.