WIZARA ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa kisekta katika kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa nchini zinapatikana karibu na wananchi na kwa ubora wa hali ya juu.
Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Maghembe jijini Dodoma wakati wa kikao cha kisekta kilichoandaliwa na Wizara ya Afya na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wanaofanya kazi na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya kilimo na Wizara ya elimu.
Dkt. Maghembe alisema lengo la kikao hicho ni kutoa taarifa ya utekelezaji wa afua mbalimbali za afya iliyofanyika sambamba na kupanga mipango kwa pamoja ya kuendelea kuboresha huduma za afya.
"Wizara ya afya inawajibika kutoa mrejesho wa wale ambayo tumekubaliana kwamba tutatekeleza yamefikia wapi ikiwemo afua za mama na mtoto, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya afya na hasa afya ya msingi pamoja na maeneo mengine". Alisema Dkt. Maghembe.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa kikao hicho kimelenga kuongea na wadau hao kuhusu vipaumbele vya Serikali ikiwemo uimarishaji wa rasilimali watu katika ya msingi, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika maeneo yote pamoja na kufikisha huduma za kibingwa kwa wananchi wa chini.
Naye Mkurugenzi wa huduma za afya, ustawi wa jamii na lishe kutoka TAMISEMI Dkt. Ntuli Kiologwe alisema kikao hicho ni cha kiufundi ambacho kiko kwenye kalenda za afya chenye lengo la kujadiliana hoja zilizoibuliwa katika kikao cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri na kuwekea mikakati mbalimbali ya utekelezaji katika kipindi cha miezi 12 ijayo.
Mwenyekiti wa wadau wa maendeleo sekta ya Afya, Getrude Mapunda alisema kikao hicho kinawapa mwanga wa mwelekeo wa Serikali kwa kuangalia utekelezaji wa miradi kwa mwaka 2021/2022 na kutafuta suluhu ya pamoja katika changamoto zilizojitokeza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.