WIZARA ya Afya imeshaanza kutumia teknolojia ya Panyabuku katika kubaini ugonjwa wa Kifua Kikuu (Tuberculosis) kwa sampuli za wagonjwa wenye dalili hizo ili kuongeza uwezo wa kutambua vimelea hivyo hasa pale ambapo njia zingine zimekuwa zimeshindwa kubaini.
Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Abel Makubi ambaye alitembelea kitengo kinachotumia teknolojia hiyo cha APOPO katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mjini Morogoro amepongeza mapinduzi kutoka kwa Wanasayansi Wazalendo ya kuwawezesha Panya buku wa Chuo Kikuu hicho kunusa na kubaini vimelea vya Kifua Kikuu katika sampuli za makohozi yanayoletwa hapo kwa ajili ya vipimo vya Kifua Kikuu, na ameelekeza kufikia mwaka huu huduma hii iweze kuzifikia zaidi ya Hospitali 100 nchini.
“Nawapongeza sana watafiti wa SUA kwa hatua ambayo mmefikia, kituo hiki baada ya kukitembelea tumeona kuwa kimekua kikifanya ugunduzi wa vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia hawa Panya. Lakini pia wameweza kuwafundisha na kusambaza hiyo Teknolojia katika nchi mbalimbali kama vile Msumbiji na Ethiopia ambako wanafanya kazi ya kupima ugonjwa wa Kifua kikuu, na kwenye nchi za Cambodia na Angola ambako wanafanyakazi ya kutambua mabomu ya ardhini”. Amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi amesema Panya hao wana uwezo mkubwa wa kugundua vimelea vya Kifua Kikuu hata kwa mtu ambaye alifanya vipimo Hospitalini kama vile vya hadubuni (microscope) na mashine za kupima vinasaba mfano GeneXpert na vipimo vingine na vikatoa majibu kuwa hana TB, lakini panya hao wana uwezo wa kubaini vimelea ambavyo mashine za Hospitalini zinaweza zisibaini. Hii inaonyesha utumiaji wa panya hawa unaweza kusaidia kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wengi zaidi. Panya mmoja anauwezo wa kugundua kama sampuli ina vimelea vya kifua kikuu kwa muda wa sekunde moja, na hupima sampuli za makohozi 100 kwa dakika 20 hivyo teknolojia hii inaweza kutumika hata kwenye upimaji wa sampuli nyingi kutoka kwenye kundi kubwa la watu (mass Screening) kwa muda mfupi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.