WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imerejesha usimamizi wa ujenzi wa miradi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ili kuongeza ufanisi zaidi kutokana na mikoa kuwa karibu zaidi na hospitali hizo.
Hayo yamesemwa jana tarehe 3 Septemba, 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Afya, Prof. Abel Makubi wakati akiongea na waandishi wa habari Jijini Dodoma.
"Kutokana na umuhimu wa kuzishirikisha Ofisi za Wakuu wa Mikoa katika utekelezaji wa miradi hiyo muhimu kwa jamii, kuanzia sasa, Wizara inarejesha jukumu la usimamizi wa utelekezaji wa miradi mingine ya Mikoa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa husika ambapo kuna miradi ya aina hiyo inayoendelea kutekelezwa," alisema Prof. Makubi.
Aliendelea kusema kuwa, Wizara itasaini makubaliano ya usimamizi wa Hospitali hizo na Makatibu Tawala wa Mikoa 'MoU' kama inavyofanyika katika Mkoa wa Katavi ili kubainisha majukumu ya usimamizi yatakayofanywa na kila upande, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi hiyo ili ianze kutoa huduma.
Aidha, alisema kuwa Wizara itahusika na kufuatilia upatikanaji wa fedha kutoka vyanzo mbalimbali na pindi fedha zitakapopatikana zitahamishiwa hazina ndogo mkoani Katavi kwa ajili ya utaratibu wa malipo ili hatua za umaliziaji wa Hospitali hiyo uendelee.
Katibu Tawala Mkoa wa Katavi ataunda Kamati zote zinazohisika na utekelezaji wa mradi kwa ngazi zote ambazo Kamati hizo ni Kamati ya ujenzi, Kamati ya Manunuzi, Kamati ya Ukaguzi na Mapokezi, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamati ya Utunzaji wa Vifaa na Kamati ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa Mradi, alisema kwa msisitizo Makubi.
Hata hivyo, Prof. Makubi aliweka wazi kuwa, fedha za utekelezaji wa mradi, kiasi cha shilingi milioni 688 tayari zipo hazina ndogo mkoani Katavi ili kuwezesha Ofisi ya Katibu Tawala kutoa malipo kwa ajili ya kuendeleza hatua za ujenzi zinazofuata.
Vile vile, Prof. Makubi alisema kuwa, Wizara imeshaandaa mahitaji halisi ya vifaa, samani, TEHAMA na wataalam, huku akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa kaeibu na Ofisi ya Mkoa wa Katavi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.