Na. Theresia Nkwanga, Dodoma
NAIBU Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameiasa Timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma inayoshiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA), kuipeperusha vema bendera ya jiji hilo akiwasisitiza kuwa na nidhamu na maadili mema itakayowasaidia katika kufikia malengo.
Hayo aliyasema katika hafla ya ugawaji vifaa vya michezo kwa timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma inayoshiriki mashindano ya UMITASHUMTA, iliyofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Dodoma.
Mavunde alisema kuwa imani yake kwa timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni kubwa akiamini kuwa itashinda kwa kishindo. “Mimi nataka mshinde michezo yote, mkawe vinara na katika mshindi wa jumla mchukue nafasi ya kwanza. Nendeni mkaipeperushe bendera ya Jiji la Dodoma, mkacheze na kutuwakilisha vizuri, muwe mfano bora, watu wajifunze kupitia ninyi. Mmepata nafasi ya kucheza, kaonesheni vipawa na vipaji vyenu, mkawe na nidhamu na maadili, muwafanye watu wawasimulie kwa mazuri, naamini mnauwezo wa kufanya vizuri sana” alisema Mavunde.
Akiwashukuru wadau waliojitolea kuhakikisha timu ya Jiji la Dodoma inakaa kambi na kuwa na vifaa bora na toshelevu vya michezo. “Nawashukuru kwa niaba ya wanamichezo wetu wadau wote mliojitokeza, Chuo Kikuu cha Dodoma, Benki ya Zanzibar na Kampuni ya NICAS kwa michango waliyoitoa kufanikisha ninyi kukaa kambini na kupata vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi 3,000,000. Siku zote huwa nafanya kwa wanafunzi wa sekondari lakini safari hii mmeniwahi mapema nimewakumbuka na wanafunzi wa shule ya msingi. Hivyo basi, namimi pia nimewaletea zawadi zangu kwaajili ya kujiandaa na mashindano” alisema Mavunde.
Naibu Waziri huyo aliwataka walimu na walezi waliochaguliwa kukaa kambini na wanafunzi wanaoliwakilisha Jiji la Dodoma katika mashindano hayo kuwalea vizuri wanamichezo hao. Alisema kuwa malezi bora kwa wanamichezo ni chachu ya ushindi ili waweze kufanya vizuri na kuipeperusha vema bendera ya Jiji la Dodoma.
Naye Afisa Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alimshukuru Naibu Waziri kwa niaba ya wanafunzi na walimu kwa kuwakabidhi vifaa vya michezo. “Kwa niaba ya wanamichezo wote, wanafunzi pamoja na walimu, nichukue nafasi hii kukushukuru Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kutukabidhi vifaa vya michezo. Vifaa hivi vitakuwa chachu katika kuwafanya wanamichezo wafanye vizuri zaidi, hatutakuangusha, tunakuahidi tutachukua vikombe vyote katika mashindano ya UMITASHUMTA” alisema Mwl. Myalla.
Aliongezea kwa kusema kuwa timu ya Dodoma Jiji imejiandaa vizuri kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA katika fani zote za michezo kuanzia ngoma, mpira wa miguu na michezo mingine. “Mwaka jana ngazi ya Taifa timu ya mpira wa miguu kutoka Mkoa wa Dodoma zaidi ya wachezaji robo tatu walitoka Jiji la Dodoma, kama mwaka jana tulitoa robo tatu ya wanamichezo wa mpira wa miguu, mwaka huu tunaimani wachezaji wa timu nzima ya mkoa watatoka wilayani kwetu. Tumechagua wachezaji wazuri sana kutoka katika shule mbalimbali na tumejipanga kufanya mazoezi ya kutosha” alisema Mwl. Myalla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.