Yaliyojiri Juni 28, 2020 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizindua mradi wa maji Wilayani Kisarawe
Aliyosema Rais Dkt. John Pombe Magufuli
Wakati nazindua mradi wa Ruvu Juu niliumia kuona Wilaya kongwe ya Kisarawe ina changamoto ya maji, ndio maana niliamua kutoa agizo kuwa maji yafike wilayani humo. Nawapongeza DAWASA kwa kuamua kuuendeleza mradi huu mpaka Pugu.
Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama, Serikali imetoa zaidi ya TZS Trilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji Vijijini ambapo upatikanaji umefikia asilimia 70.1 na Mijini ni asilimia 84.
Jumla ya TZS Bilioni 17.25 imetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, natoa agizo la kujengwa barabara ya lami kutoka Kisarawe hadi mbuga ya Nyerere kwani hatuwezi kuwa na mbuga kubwa tena yenye jina la Baba wa Taifa halafu kusiwe na barabara.
Naupongeza Mkoa huu kwa kuendelea kufungua uchumi, mmeongeza viwanda kutoka 395 mwaka 2016 hadi 1,192 mwaka 2020 ambavyo vimetoa ajira za moja kwa moja takribani 30,000.
Natoa agizo kwa viongozi wa Wilaya ya Kisarawe kuangalia upya suala la stendi mpya ili kuondoa changamoto zilizopo, suala la barabara ya kutoka Kisarawe kwenda Kibaha nimelichukua.
Natengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe kwa kufanya mambo ambayo hayaendani na maadili ya kazi yake, nawaagiza viongozi husika kumpangia kazi ya chini ambayo ana uwezo nayo na asifanye wilayani hapa.
Rais Dkt. John Magufuli amemteua aliyekuwa Afisa Tawala wa Wilaya ya Kisarawe, Mwanana Msumi kuwa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo baada ya kutengua uteuzi wa Katibu Tawala aliyekuwepo.
Alichosema Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja
Hali ya upatikanaji wa maji kwa Pwani ni nzuri, Vijijini ni 66.6 na Mijini ni 88, DAWASA inaendelea na miradi takriban minne na Wizara ya Maji imekamilisha mradi mkubwa katika Kisiwa cha Jibondo.
Mradi wa maji kutoka Kibamba hadi Kisarawe unaozinduliwa leo umegharimu TZS Bilioni 10.6, mradi huu una awamu ya pili ambayo itagharimu TZS Bilioni 7.3, awamu hii imeshaanza.
Mradi huu umetokana na maelekezo yako Rais Magufuli uliyoyatoa mnamo mwaka 2017 wakati ukizindua mradi wa maji Ruvu Juu, mradi huu umetekelezwa kwa miezi 14.
DAWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa 28 inayogharimu TZS Bilioni 56 na miradi 526 imekamilika kwa gharama ya TZS 11.4 pia tumeongeza ajira kutoka 850 mwaka 2015 hadi 2,150 mwaka 2020.
Lengo la DAWASA ifikapo mwaka 2025 ni kuhakikisha wananchi wote wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam wanapata maji safi na salama.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.