Na. Abdul Juma, MIYUJI
Wananchi wa Mtaa wa Mpamaa, Kata ya Miyuji jijini Dodoma, wameeleza kufurahia kwao maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika Zahanati ya Mpamaa kuanzia ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba na usimikaji wa mfumo wa Tehama yamerahisisha upatikanaji wa huduma na kuboresha mazingira ya kufanyika kazi.
Katika mahojiano na wanahabari waliotembelea zahanati hiyo kwa ajili ya kufuatilia maboresho yaliyofanywa katika zahanati hiyo wananchi walielezea kufurahia maboresho hayo na huduma zinazotolewa.
Mkazi wa Mtaa wa Mpamaa, Anifa Sagika alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwajengea zahanati ya Mpamaa. “Hapo awali, tulikosa huduma muhimu, hasa sisi akina mama wajawazito tulilazimika kutembea umbali mrefu au kujifungulia nyumbani. Sasa tuna huduma inatolewa karibu nasi” alisema Sagika.
Nae Malimi Charles alisema kuwa anapongeza juhudi za serikali kuhakikisha huduma za afya zinapatikana katika kata hiyo. Alisema kuwa zahanati hiyo imesaidia kupunguza vifo vya wajawazito na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya na kumtaja Rais Samia kuwa ametimiza ndoto ya muda mrefu ya wakazi wa Miyuji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpamaa, Happy Joshua, alieleza namna mradi huo ulivyotekelezwa kwa mafanikio. “Ninamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake. Pia nawashukuru Mbunge wetu wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, na Diwani wetu Beatrice Ngerangera kwa kushirikiana kuleta maendeleo. Zahanati hii imesaidia sana, hasa kwa huduma za mama na mtoto ambazo zamani zilifanyika chini ya mti katika kanisa la RC” alisema Joshua.
Afisa Tabibu na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mpamaa, Dkt. Fatuma Maseli, alisema kuwa zahanati hiyo ilipokea fedha Shilingi Milioni 43 kwa ajili ya ununuzi wa samani, vifaa tiba, pamoja na kuwekewa mfumo wa kidigitali unaorahisisha utoaji wa huduma. “Awali wagonjwa walikuwa wanakaa chini kwa kukosa viti, lakini sasa tuna mazingira bora. Pia tumepatiwa kichomea taka hatarishi na mfumo wa kisasa unaoitwa ‘Gothomis’. Tunawapongeza viongozi wetu na tunaomba Mungu azidi kuwabariki,” alisema Dkt. Maseli.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.