Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KITUO cha Afya Chang’ombe kinatarajia kuhudumia wakazi wapatao 25,000 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuwapunguzia adha wananchi ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.
Kauli hiyo ilitolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa akitoa taarifa fupi ya Kituo cha Afya Chang’ombe kwa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyoongozwa na Mkurugenzi wake, Joseph Mafuru kutembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki.
Dkt. Method alisema kuwa Kituo cha Afya Chang’ombe kinatarajia kuhudumia wananchi 25,000 kitakapokamilika. Alisema kuwa Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi 250,000,000 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa majengo mawili na kichomea taka. Alisema kuwa majengo mawili yaliyojengwa ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na jengo la maabara. Kiongelea ujenzi wa kichomea taka, alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika baada ya wiki moja.
Mganga mkuu huyo aliishukuru serikali kwa uamuzi huo wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Alisema kuwa eneo lote la Kata ya Chang’ombe pamoja na ukubwa wake halikuwa na kituo cha afya cha serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha afya ni hatua nzuri kwa maboresho ya huduma za afya wananchi wa Kata ya Chang’ombe. “Kata ya Chang’ombe ina wananchi wengi. Hivyo, ujenzi wa kituo cha Afya ni uamuzi wa kimkakati katika kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilifanya ziara ya kazi kutembelea vituo vya afya vya Chang’ombe, Kizota na Nkuhungu kuona hali halisi ya utekelezaji wa ujenzi unaoendelea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.