MKUU wa Wilaya ya Dodoma Mjini Josephat Maganga leo ameendelea na ziara yake ya kujitambulisha kwa wananchi wa Wilaya anayoiongoza kwa kutembelea Kata ya Chahwa ambayo ni miongoni mwa Kata 41 zinazounda Jijini la Dodoma.
Akiongea na wananchi hao Mheshimiwa Maganga amesema "Pamoja na kujitambulisha, nimekuja pia kuangalia miradi ya wananchi ambayo inaendelea hapa Chahwa na tatu kuongea na wananchi kwa maana ya wananchi kutoa kero zao ili zishughulikiwe"
Akifafanua zaidi Mhe. Maganga aliwaomba wananchi waliojitokeza waweze kuongea ili aweze kufahamu maendeleo yao na kusikia kero ama mambo ambayo si mazuri na yanayohitaji kuondolewa.
"..tena mna bahati kubwa sana, mko karibu na ukuta wa Ikulu hapa na mnafahamu nani yuko huko Mhe. John Pombe Magufuli, siku zote ametuelekeza sisi wasaidizi wake tuwe karibu na wananchi wetu, tujue kero zao" alisisitiza Mhe. Maganga akiwapa tumaini wananchi hao.
Naye Alfa Malogo mwananchi wa Chahwa akichangia katika mkutano huo wa hadhara akatoa kero inayohusu maeneo ya wazi. "Mhemishimiwa Mkuu wa Wilaya hapa tumegawanyika makundi mawili, kuna watu ambao hawana ardhi lakini wanapotosha watu, ujue kuwa hawa wapimaji (wa Jiji la Dodoma) wanaongea ukweli.
Kuna maeneo ya wazi hapa Chahwa tunayajua, ... hawa viongozi wajumbe kuna maeneo kama saba ambayo tunayajua wamegawana hawa viongozi" alihitimisha Malogo kwa msisitizo mkubwa.
Mwananchi mwingine mwanamke ambaye hakutaja jina lake alimuomba Mkuu wa Wilaya asaidie eneo la Chahwa kupata umeme na shule ya sekondari.
"Tunaomba tupatiwe umeme ili wanawake tuweze kuutumia kufanya biashara hata za kutengeneza 'ice cream' na kujipatia kipato, pili tunaomba shule ya sekondari. Watoto wetu wamekuwa wakisoma maeneo ya mbali kama Mtumba, Msanga, Hombolo, Ipala na Mahoma, na sisi tupatiwe shule ya sekondari ya Kata" alisema mama huyo na kushangiliwa na wananchi waliojitokeza katika mkutano huo wa hadhara.
Akijibu hoja na kero zilizowasilishwa, Mhe. Mkuu wa Wilaya alitoa ufafanuzi kuwa, katika ardhi ndiyo mipango yote ya Serikali inafanyika, kama kuna uhitaji wa barabara, majosho ya kuoshea ng'ombe, reli na kadharika tunajenga kwenye ardhi.
"...ardhi pia ni uchumi, watu wanauza ardhi kupata pesa, watu ambao ardhi yao inatwaliwa kwa matumizi mengine wanalipwa pesa, ...ardhi ina mazuri, ina fujo na ina vurugu nyingi ambazo zinaweza kuepukika kama kuna mipango mizuri, lakini pia inaweza kuleta madhara kama kuna mipango mibaya" alifafanua Mhe. Maganga.
Akielezea zaidi, Mhe. Maganga alisema kuwa, kutokana na watu kuongezeka na ardhi kutoongezeka, suala la ardhi lote limewekewa sheria kwa malengo ya kutaka watu waishi vizuri na kwa amani na hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria.
"Maeneo yote yaliyotambuliwa kwa matumizi ya umma soko, mabwawa, mpira, chanjo zote, banio la ng'ombe, lambo la serikali na kadharika, waliojimilikisha maeneo hayo waondoke mara moja, Mkurugenzi, hii ni kazi yako toa notisi hawa watu waondoke kwenye maeneo hayo wayaache" alimalizia Mkuu huyo wa Wilaya kwa agizo la wahusika kuondoka mara moja.
Wananchi wa Kata ya Chahwa jijini Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Josephat Maganga (hayuo pichani) wakati wa mkutano wa hadhara katani hapo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.