TAASISI ya Maendeleo ya Vijana Mkoani Dodoma – DOYODO ilifanya ziara ya kutembelea Baraza la Vijana Zanzibar na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa lengo la kujifunza namna vijana wanavyoshirikishwa katika ngazi za maamuzi ikiwemo ushiriki wa vijana katika Baraza la Wawakilishi.
Ziara hiyo iliwajumuisha Afisa Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Idara Kuu ya Maendeleo ya Vijana, Atupokile Mhalila, Afisa Vijana Mwandamizi Mkoa wa Dodoma, Tumsifu Mwasamale, Mkurugenzi Mtendaji wa DOYODO, Rajabu Juma Suleman, Meneja Miradi wa DOYODO, Charles Ruben na wawakilishi wa vijana wawili.
Mkurugenzi Mtendaji wa DOYODO, Rajabu Juma Suleiman alipata wasaa wa kufanya mazungumzo na mmoja wa Wawakilishi wa Baraza hilo kutoka Jimbo la Mwera Mhe. Mihayo N’hunga ambaye alielezea kuwa asilimia kubwa ya Wajumbe Baraza la Wawakilishi na Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni vijana ambapo pia alifafanua namna Baraza hilo linavyotoa fursa kwenye Baraza la Vijana Zanzibar.
Fursa zingine ambazo Baraza la Vijana Zanzibar ambalo lilianzishwa mwaka 2015 linazozitoa kwa vijana ni pamoja na kuanzisha miradi ya maendeleo, miongoni mwa miradi iliyoanzishwa ni Miradi ya Ufugaji Kuku, Kilimo cha kitalu nyumba (Green House) na ushonaji.
Aidha, Baraza hilo limejikita katika kuwapatia vijana fursa za kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi hususani vikao vya bajeti za maendeleo.
Vile vile kuna mradi wa Redio ya Kati FM ambao ulifadhiliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mwaka 2019 wakati huo akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile ipo miradi ya Usafi wa Miji inayoendeshwa na vijana.
Timu hiyo ilipata nafasi ya kujifunza mengi juu ya Baraza la Vijana Zanzibar na umuhimu wake kwa jamii. Timu hiyo ilielezwa kuwa Baraza la Vijana Zanzibar limegawanyika katika ngazi tatu ambazo ni Baraza la Vijana Taifa, Baraza la Vijana Wilaya na Baraza la Vijana Shehia.
Chanzo: Idara ya Habari na Mawasiliano - DOYODO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.