MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde amekagua miundombinu ya barabara na nyumba zilizobomoka katika kata ya Zuzu kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Jiji la Dodoma na kujionea mwenyewe uharibifu mkubwa uliojitokeza.
Akitoa taarifa, Diwani wa kata ya Zuzu Mhe. Awadh Abdallah akiwa pamoja na Mtendaji wa Kata Mabrouk Seif, amebainisha kwamba wananchi takribani 286 nyumba zao zimepata uharibifu hali ambayo imepelekea wengi kukosa makazi ya kudumu na kupoteza mali nyingi pamoja na vyakula huku miundombinu ya barabara ikiwa imeharibiwa kwa kiwango kikubwa.
Akiongelea hali hiyo Mhe. Mavunde alisema, "Nimekuja kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua na pia kuwapa pole wananchi ambao nyumba zenu zimebomolewa na mvua hizi, niwaombe wananchi tuendelee kuchukua tahadhari kutokana na mvua hizi ili zisilete madhara zaidi. Nitaendelea kuwa pamoja nanyi kutatua changamoto zinazowakabili hasa katika kipindi hiki na leo nimewaletea unga wa sembe tani 1 magunia ya maharage na maji".
Wananchi wa kata ya Zuzu wamemshukuru Mbunge Mavunde kwa namna anavyojitoa katika matatizo ya wananchi wa jimbo lake na kuwajali katika shida zao kwa kuwapatia misaada ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwapunguzia changamoto za mahitaji ya chakula na makazi katika kipindi hiki.
Tazama picha za matukio mbalimbali za ziara ya Mbunge Anthony Mavunde katika kata ya Zuzu:
Diwani wa kata ya Zuzu Awadh Abdallah akitoa taarifa ya madhara yaliyowakumba wananchi wa Zuzu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dodoma, kulia ni Mabrouk Seif, Mtendaji wa kata ya Zuzu.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mhe. Anthony Mavunde akiongea na wananchi wa Zuzu, alipowatembelea ili kuwapa pole na kutoa misaada kwa wananchi hao.
Mheshimiwa Mavunde akingalia baadhi ya nyumba zilizoathirika na mvua na kusababisha adha kwa wananchi wa Zuzu.
Viroba vya unga kiasi cha tani moja ambao Mhe. Mavunde ametoa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Zuzu walioathirika na madhara ya mvua.
Mheshimiwa Mavunde akiwaaga wananchi wa Zuzu baada ya kuwatembelea kwa lengo la kuwapa pole na kutoa misaada ya kijamii.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.