KITUO cha Afya Makole kimetembelewa na Mshauri wa Mifumo ya Taarifa za Afya kutoka Shirika la Misaada la watu wa Marekani (USAID) Bi. Joy Kamunyori, aliyeambatana na Mshauri wa Mifumo ya Afya kutoka USAID-Tanzania, Makunda Kassongo, wataalam kutoka mradi wa PS3 Plus na timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Mshauri huyo alifika kituoni hapo kuona matumizi ya Mfumo Madhubuti wa Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo vya kutolea Huduma za Afya (GOTHOMIS) na Mfumo wa Uhasibu na Utoaji wa Taarifa za Fedha kwa ngazi ya Vituo cha Kutolea Huduma (FFARS).
Matumizi ya mfumo wa GoTHOMIS yamesaidia kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na utoaji huduma, aidha matumizi ya mfumo wa FFARS yamesaidia kuboresha usimamizi wa fedha na matumizi yake katika kituo cha Makole.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method, mbele ya wageni hao kwenye ziara yao kuona namna mifumo hiyo inavyosaidia katika utendaji kazi na utoaji huduma katika vituo vya afya.
Method alisema kuwa kabla ya kufunga mfumo wa GOTHOMIS, Kituo cha Afya cha Makole kilikuwa kinahudumia wateja 108,000 kwa mwaka (2017/18), kwa sasa kituo kinahudumia wateja 300,000 kwa mwaka (2021/22) ikiwa ni ongezeko la asilimia 227 sambamba na hilo kumekuwa na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato kutoka Shilingi million 84 kwa mwaka 2017/18 hadi kufikia Milioni 373 kwa mwaka wa fedha 2021/22, ikiwa ni ongezeko la asilimia 444.6 kwa kipindi cha miaka mitatu.
“Mfumo wa GOTHOMIS toleo la 4, unamuwezesha mgonjwa anapofika kituoni kusajiliwa kieletroniki na kufuatiwa na hatua zingine za matibabu kwa njia ya mfumo ikiwemo huduma za vipimo vya maabara, kuonana na daktari, kupata dawa, kulazwa na kadharika. Uwepo wa mfumo katika kituo chetu cha afya umesaidia kuongezeka kwa kasi ya utoaji huduma bora na ukusanyaji wa mapato.
Katika ukusanyaji wa mapato Kituo cha Afya Makole yameongezeka kutoka shilingi milioni 84 kwa mwaka 2017/18 hadi kufikia shilingi milioni 373 kwa mwaka wa fedha 2021/22 hilo ni ongezeko la asilimia 444.6 katika kipindi cha miaka mitatu.”
Akiongelea zaidi mafanikio ya mfumo huo, Mganga Mkuu Dkt. Andrew Method amesema kuwa mfumo umeongeza usiri wa taarifa za wagonjwa, umerahisha madaktari kuhudumia watu wengi zaidi, umesaidia upatikanaji wa taarifa mbalimbali, unaweza kutoa taarifa za utendaji kazi kwa kila mtumishi, umepunguza muda wa wagonjwa kusubiri huduma, unatoa takwimu sahihi za wagonjwa na dawa, na usimamizi wa matumisi ya dawa.
Aidha, akiongea na tovuti hii Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Uhusiano, Joseph Fungo alifafanua kuwa kitengo chake kinatoa msaada wa kitaalamu wa matumizi ya mifumo hiyo katika vituo vya afya 3 ambavyo tayari vimesimikwa mfumo wa GoTHOMIS ambavyo ni Makole, Mkonze na Hombolo.
“Katika kitengo changu cha TEHAMA baada ya kufunga mfumo wa GoTHOMIS katika vituo vya afya 3 kati ya 4 tulivyonavyo tuliwapatia mafunzo watumishi wote kuhusu matumizi ya mfumo huu, na ikitokea changamoto yoyote huwa tunapewa taarifa mapema na wataalamu wangu wanafika eneo husika na kushughulikia changamoto husika kwa wakati” alisema Fungo.
Hata hivyo, Afisa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Baraka Samson alipokea na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika mfumo huo ikiwemo kujaa mapema sehemu ya kuhifadhia taarifa za matibabu ya wagonjwa na kushuka kwa kasi ya mtandao katika baadhi ya maeneo.
“Sisi upande wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI tumepokea changamoto hizo na tutazifanyia kazi kwa haraka ili huduma iweze kuongezeka kwa kasi na kuwa bora zaidi” alisema Samson.
Bofya hapa kuona: PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.